Yanga yatangulia CAF

SARE iliyopata Simba dhidi ya Namungo na kichapo ilichopewa Azam FC kutoka kwa Kagera Sugar, imewarahisishia kazi Yanga, kwani vinara hao wa Ligi Kuu Bara imekuwa klabu ya kwanza ya Tanzania kujihakikishia tiketi ya michuano ijayo ya CAF.

Yanga imefunga hesabu mapema ikiwa imesaliwa na mechi nane mkononi baada ya jana kucheza mchezo wa 22 dhidi ya Ruvu Shooting mjini Kigoma, ikiwa imekamata tiketi ya michuano ya kimataifa ya msimu ujao.

Simba ililazimishwa sare ya 2-2 na Namungo FC kwenye Uwanja wa Ilulu, Lindi wakati Azam ilichapwa 1-0 na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, Kagera katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu inayoelekea ukingoni. Sare dhidi ya Simba iliifanya Namungo ikomalie nafasi ya tatu ikifikisha pointi 30 huku Azam ikisalia nafasi ya nne na alama 29, lakini kabla ya mechi dhidi ya Ruvu. Yanga ina pointi 56 zinazowapa jeuri ya kumaliza ndani ya Tatu Bora. Pointi ilizonazo Yanga zinaweza kufikiwa na timu za Simba, Azam, Kagera Sugar, Mbeya City na Geita Gold tena hapo ni lazima zishinde mechi zilizosalia, vinginevyo huenda baadhi zikakamiwa kuzigusa kabla msimu haujafungwa mwezi ujao.

Ofisa habari wa Yanga, Hassan Bumbuli alisema kinachotokea ni matunda ya maandalizi na mikakati waliyoweka kutimiza malengo yao.

“Siri ya mafanikio ni juhudi za pamoja za wadhamini wetu hasa GSM, uongozi, wachezaji, benchi la ufundi, wanachama na mashabiki katika kutimiza malengo tuliyojiwekea msimu huu hasa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la Azam,” alisema.

“Tuna kikosi bora ambacho kinaweza kutufanya tutimize malengo yetu.”

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii