Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenksyy amesema kuna changamoto kubwa ya upatikanaji wa huduma za matibabu na dawa katika maeneo ya mashariki na kusini yanayodhibitiwa na Urusi nchini Ukraine. Zelenksyy amesema hakuna matibabu yanayowafikia wagonjwa hasa wa saratani na kwamba dawa za kupambana na maambukizi kutokana na bakteria pia ni chache. Amesema hali hiyo imewanyima fursa madaktari kuwahudumia wagonjwa au kuwafanyia upasuaji.Katika hotuba yake ya kila siku kwa njia ya video, Rais huyo wa Ukraine ameongeza kuwa, wakati wa vita hivyo jeshi la Urusi limerusha makombora 2,014 katika ardhi ya Ukraine huku ndege za kivita za Urusi zilizorekodiwa katika anga ya Ukraine zikiwa 2,682. Amesema miundombinu na majengo yaliyoharibiwa katika vita hivyo ikiwemo hospitali na vituo vyengine vya matibabu inakaribia 400.