WAJASILIAMALI WAHIMIZWA KUTENGENEZA BIDHAA ZENYE UBORA ILI KULINDA SOKO

Na Mwandishi Maalum, Mwanza

Wajsasiliamali wametakiwa kuendelea kuboresha bidhaa zao ili kudhibiti soko la nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na hatimaye Afrika nzima, hususan katika kipindi hiki Bara la Afrika limeanzisha Soko Huru la Biashara (CfTA).

Hayo yamesemwa tarehe 4 Desemba 2021 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama (Mb) ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika Siku ya Tanzania kwenye Maonesho ya 21 ya wajasiliamali ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yanayofanyika jijini Mwanza kuanzia tarehe 2 hadi 12 Desemaba 2021.



“Nimetembelea mabanda ya wajasiliamali na kushuhudia bidhaa zenye ubora wa hali ya juu. Hivyo, tuendelee kuboresha bidhaa zetu ili tuingie masoko mengine badala ya kutegemea soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki pekee”, Waziri Mhagama alisema.

Waziri Mhagama alitoa ahadi kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi nyingine za Jumuiya, kuimarisha maonesho hayo ili yaweze kupanua soko, kuongeza ajira, kukuza uchumi na hatimaye kuondoa umasikini kwa raia wa nchi wanachama wa EAC.

Maonesho hayo ambayo yatafunguliwa rasmi tarehe 5 Desemba 2021 na Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo (Mb) kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan yanapambwa na shughuli mbalimbali zikiwemo mafunzo kwa wajasiliamali yenye mada tofauti tofauti kama vile; vikwazo visivyo vya kibiashara, wepesi wa kufanya biashara ndani ya Jumuiya, fursa za biashara katika nchi ya Sudan Kusini, UVIKO-19 na biashara na namna ya kusafirisha bidhaa baina ya nchi za Jumuiya.

Mada hizo zinazowasilishwa na wabobezi kutoka sekta mbalimbali, zikiwemo Wizara ya Viwanda na Biashara, Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na taasisi zinazosimamia urasimishaji wa bidhaa, kwa siku ya tarehe 4 Desemba 2021, wajasiliamali wamejifunza falsafa ya Kaizen ambayo inahimiza umuhimu wa mjasiliamali kuboresha utendaji wake kila siku katika maeneo yote kama ya ubunifu, utafutaji wa masoko, vifungashio, utoaji wa huduma kwa mteja n.k.

Mkurugenzi wa Biashara na Forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Bw. Keneth Bagamuhunda alieleza namna maonesho hayo yanavyondelea kuimarika mwaka hadi mwaka na kubainisha kuwa maonesho ya mwaka huu yameandaliwa vizuri na washiriki wamekuwa wengi zaidi ukilinganisha na miaka mingine.

Wajasiliamali zaidi ya 900 wanashiriki maonesho hayo wakiwemo 420 wa Kitanzania kutoka maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Zanzibar. Aidha, viongozi wa Serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Mhandisi. Robert Gabriel Luhumbi; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Zanzibar, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mhe. Mudriki Soragha; Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Vijana, Kazi na Ajira, Mhe. Patrobas Katambi; Waziri wa Jiji la Kampala, Hajatti. Minsa Kabanda; wabunge wanne kutoka Uganda waliungana na Mhe. Mhagama katika Siku ya Tanzania kwenye maoesho hayo.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii