Takriban watoto elfu 2 walifariki Tigray kutokana na utapiamlo

Karibu watoto 1,900 chini ya umri wa miaka 5 wamefariki kutokana na utapiamlo katika eneo la Tigray katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Haya ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na maafisa wa afya wa eneo hilo na ulioonekana na shirika la habari la Associated Press. Vifo hivyo vinaripotiwa kurekodiwa katika taasisi za afya kote Tigray kati ya Juni mwaka jana na Aprili mosi mwaka huu. Eneo la Tigray Magharibi ambalo liko chini ya udhibiti wa majeshi kutoka eneo jirani la Amhara, halikujumuishwa katika utafiti huo. Daktari aliyeshiriki utafiti huo amesema huenda idadi ya watoto waliofariki kutokana na utapiamlo ikawa juu zaidi kwa kuwa wazazi wengi hawawapeleki watoto wao katika taasisi za afya kutokana na changamoto za usafiri. Daktari huyo amesema vifo vingi vinavyotokana na njaa haviwekewi takwimu.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii