Waziri Mkuu Uingereza katika kiti moto

Waziri Mkuu Boris Johnson kwa mara ya kwanza atakabiliana na wabunge wenye hasira tangu atozwe faini kwa kuvunja sheria, wakati kashfa ya sherehe itakapoendelea kumzonga.

Kiongozi huyo wa Uingereza alipangua bomu la kwanza baada ya kupigwa faini kwa kuvunja sheria za kudhibiti maambukizi ya Ugonjwa wa Virusi vya Corona (Covid-19) katika hafla iliyofanyika mwaka 2020, akikataa kujiuzulu.

Lakini Johnson anategemea siku chache ngumu wakati bunge la makabwela litakapoanza tena baada ya mapumziko ya Pasaka, huku wabunge wakitaka kujua sababu za kiongozi huyo kusisitiza mara kwa mara kuwa hakuna kanuni zilizovunjwa.

Kujua kuwa unalidanganya bunge ni kuvunja kanuni za uongozi za serikali, ambazo zinasema mkosaji anatakiwa ajiuzulu, na viongozi wa upinzani wamepania aondoke.

Hata hivyo, licha ya kuwa kiongozi wa kwanza wa zama za sasa kupigwa faini kwa kuvunja sheria na kuwepo uwezekano wa polisi kuchunguza matukio zaidi ya uvunjaji sheria katika ofisi ya Downing Street, waziri huyo mkuu anaonekana kuendelea na mambo kama kawaida.

Johnson, mwenye miaka 57 ameripotiwa kujaribu kujiweka kando na sakata hilo kwa kuendelea na shughuli zake kama kawaida, ikiwemo ziara ya siku mbili nchini India keshokutwa (Alhamisi).

"Waziri mkuu atazungumzia upande wake... na tutamuorodheshea matukio kwa jinsi tunavyojua na kumuulizwa maswali na wabunge," waziri wa serikali, Greg Hands aliiambia Sky News jana (Jumatatu).

"Anaendelea na kazi, amefanikiwa na serikali imefanikiwa kwa kila kitu kutoka katika programu ya uchanjaji kwa msaada mkubwa wa Ukraine."

Polisi wa Metyropolitan wa London wanachunguzamatukio kadhaa ya tuhuma za ukiukwaji wa sheria za kudhibiti maambukizi ya Covid-19 yaliyofanywa na Johnson na wafanyakazi wake wa ikulu, ambako anaishi na kufanya kazi wakati wa ugonjwa huo.

Polisi walisema wiki iliyopita kuwa maofisa wake wameshatoza zaidi ya faini 50.

Kashfa hiyo, ambayo ni mpya miongoni mwa nyingi zilizomkumba Johnson tangu katikati ya mwaka jana, imesababisha cheo chake kiwe shakani na wabunge wa Conservative wako katika hali ya uasi.

Lakini ameimarisha uwezekano wa kubakia madarakani kutokana na jinsi alivyoshughulikia vita nchini Ukraine, ambayo iliwafanya waache kumkodolea macho katika kipindi ambacho angeweza kuondolewa.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii