Kamishina wa haki za binadamu katika serikali ya Ujerumani Luise Amtsberg ametaka wakimbizi wanaoingia Ujerumani kutoka mataifa kama Afghanistan na Syria wapewe haki sawa na wakimbizi wanaotokea Ukraine. Akizungumza na gazeti la "Neuen Osnabrücker" Amtsberg amesema wakimbizi kutoka Ukraine wanapewa fursa nyingi sana nchini Ujerumani. Wakimbizi wa Ukraine nchini Ujerumani, kinyume na wakimbizi wengine, wanaweza kuishi wanapotaka na moja kwa moja wanaweza kufanya kazi. Na sasa Amtsberg anasema ukosefu huo wa usawa kwa wakimbizi umetokana na miaka ya sera mbaya. Ametoa wito kwa serikali ya muungano iliyoko madarakani sasa kuyafanyia mabadiliko yote hayo.