Bi Zainab alituma katika mtandao wake wa Twitter siku ya Jumamosi masaibu aliyoyapata katika moja ya hoteli karibu na ufukwe eneo la Nungwi visiwani humo.
Katika taarifa yake anaeleza kuwa alinusurika kubakwa na mtu ambaye aliingia kwenye chumba chake cha hoteli majira ya usiku. Mtu huyo ambaye alikua akizungumza Kiswahili hakufanikiwa kufanya kitendo hicho baada ya yeye kumtishia kuwa ana HIV.
Anaendelea kueleza kuwa baada ya mtu huyo kuondoka alifanikiwa kukimbia na kupata hifadhi kwa wageni wengine. Na aliporudi asubuhi alikuta pesa zake zaidi ya dola 1000 zimeibiwa.
Katika taarifa yake Zainab alieleza kuwa tukio hilo lilitokea mwaka mmoja uliopita na alikaa kimya huku akipatiwa msaada wa ushauri nasaha kabla ya kueleza tukio hilo siku ya jana.
HANZO
Bi Zainab ni raia kutoka Nigeria, kwa mujibu wa mtandao wake wa Instagram Zainab ni mkemia ambaye ana shahada ya kemia lakini pia ni mfanyabiashara.
Mwezi Aprili mwaka jana alifika Zanzibar kutalii pamoja na kusherehekea siku yake ya kuzaliwa kabla ya tukio hilo kumtokea usiku wa kuamkia siku ya kumbumbuku yake kuzaliwa.
Baada ya taarifa hii kusambaa kwa kasi katika mitandao ya kijamii, Kamisheni ya Utalii Zanzibar kwa niaba ya Wizara ya Utalii ilisema kuwa imesikitishwa sana na taarifa hiyo na wameanzisha uchunguzi wa tukio hilo.
Katika taarifa hiyo Kamisheni imesema kuwa baada ya uchunguzi watatoa taarifa kamili na kuwa vitendo vya uhalifu kwa watalii havikubaliwi.
Naye Waziri wa Biashara na Maendeleo ya viwanda Zanzibar, Omar Said Shaaban, akizungumza katika mjadala kupitia Twitter alisikitishwa na tukio hilo na alisema kuwa serikali ya Zanzibar inafuatilia kwa makini tukio hilo na kukusanya ushahidi kutoka maeneo husika.
''Nilikuwa na mazungumzo na Waziri wa uUtalii ambaye yupo safarini, na Kamishna wa Utalii, na wamesema kuwa wanalifuatilia hili kwa kina, na tunafanya jitihada na kuwasiliana moja kwa moja na dada Zainabu ili kujua kilichotokea kwa undani'' Alisema Omar.
Kwa upande wa polisi, hawajatoa taarifa yoyote kuhusu tukio hilo.
Hoteli inayodaiwa kutokewa kwa tukio hilo lilimetokea, imetoa taarifa kadhaa kupitia mitandao yake ya kijamii, lakini katika utoaji wa taarifa hizo baadhi zimekua zikifutwa na kurudiwa.
Katika taarifa yake ya awali, hoteli hiyo ilieleza kuwa tukio lilitokea mwezi Aprili mwaka jana na utaratibu wa kufikishwa polisi ulifanyika, kisha kwenda Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na baadaye Ofisi ya Makamu wa Rais. Lakini mlalamikaji Zainab alikataa kuendelea na kesi.
Iliongeza pia kuwa mfumo wao wa mtandao ulidukuliwa.
Hata hivyo hoteli hiyo ilifunga baadhi ya mitandao yake ya kijamii, na tovuti yao haipatika.
Mjadala mkali umeendelea katika mitandao ya kijamii kutoka nchi mbalimbali za Afrika.
Mambo kadhaa yameibuka katika mjadala huu, ikiwemo makundi ya watu wenye pande tofauti, wale wanaotaka haki kutendeka na wale wanaohitaji upande mwingine wa simulizi.
Katika taarifa ya Zainab, alianisha mambo kadhaa ikiwemo picha na video za hoteli, maafisa wa polisi pamoja na kituo cha polisi eneo la Nungwi.
Taarifa za hoteli bado zina utata kutokana na kubadilika na kufutwa kwa baadhi ya maelezo.
Kwa upande wa Ubalozi wa Nigeria nchi Tanzania bado haujatoa taarifa yoyote kuhusu tukio hilo.
Uchunguzi wa tukio hilo unaofanywa na mamlaka visiwani Zanzibar bado unaendelea.
Tukio kubwa lililongonga vichwa vya habari kutoka visiwani Zanzibar ni lile la watalii wawili kutoka Uingereza kumwagiwa tindikali.
Tukio hilo lilisababisha ulinzi kuimarishwa na vifaa vya CCTV kufungwa katika maeneo mbalimbali ya eneo la Stone town.
Zanzibar inategemea sana pato la utalii, kwa mujibu wa mamlaka visiwani humo mwaka 2021 Zanzibar ilikusanya bilioni 69.1 sawa na dola za marekani milioni 29.893 kutoka katika shughuli za kitalii pekee.