MAJESHI ya Ukraine ambayo yapo jijini Mariupol yamegoma kujisalimisha kama ilivyotolewa amri na Urusi na badala yake yameapa kupambana hadi mwisho kutetea mji huo ambao upo mashariki mwa nchi ya Ukraine.
Mapema hivi karibuni serikali ya Urusi ilitoa masaa saba kwa wanajeshi wa Ukraine waliosalia katika mji wa Mariupol kukata tamaa na kujisalimisha lakini wanajeshi hao wamegoma hiyo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri Mkuu wa Ukraine Denys Shmyhal.
Kwa upande mwingine Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema Ukraine haikuwa na mpango wa kuachia eneo lolote lililopo Mashariki mwa jimbo la Donbas.
Kwa wiki za hivi karibuni Urusi imeelekeza nguvu zake kwa majimbo yanayopatikana mashariki mwa Ukaraine.
Taarifa ya Ukraine inadai watu watano wamefariki baada ya mashambulizi ya Urusi kwenye Jiji la Kharkiv na wengine wawili wameripotiwa kupoteza maisha katika shambulio la mji wa Zolote.
“Mji bado haujachukuliwa na Urusi, bado kuna majeshi yetu kule kuna askari wetu kwahiyo watapambana hadi mwisho na kwasasa bado wapo kwenye Jiji la Mariupol.”
Jiji la Mariupol linachukuliwa kama Jiji la kimkakati ambalo likikamatwa na majeshi ya Urusi litaiunganisha Crimea na majimbo yaliyojitenga ambayo yanaunga mkono uhudi za Urusi kuivamia Ukraine.