Ujerumani kupeleka vifaru nchini Ukraine

 Marekani imeongoza jana mkutano wa zaidi ya nchi 20 katika kituo cha jeshi la anga la Marekani cha Ramstein magharibi mwa Ujerumani na kujadili kuhusu kuimarisha ulinzi wa Ukraine wakati inapopambana na uvamizi wa Urusi. Washirika kadhaa waliutumia mkutano huo kutoa ahadi za msaada kwa ajili ya jeshi la Ukraine katika kipindi kizima cha vita na baada ya kumalizika kwa vita hivyo. Katika mkutano huo, Ujerumani ilitangaza kuwa itapeleka vifaru Ukraine. Tangazo hilo ni mabadiliko makubwa ya sera yake kuhusu upelekaji wa zana za kijeshi nchini humo. Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin amesema “mataifa kote ulimwenguni yanasimama pamoja katika kuiunga mkono Ukraine na katika vita vyake dhidi ya uchokozi wa Urusi.” Austin aliongeza kuwa mkutano huo utakuwa unafanyika kila mwezi ili kujadili jinsi Ukraine inavyoweza kujilinda. Marekani na washirika wake wametoa vifaa vya thamani ya zaidi ya dola bilioni 5 kusaidia ulinzi wa Ukraine tangu vita hivyo vilipoanza.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii