WarsawUkraine imeituhumu Urusi kuwa inaihujumu Ulaya kwa kusitisha usambazaji wa gesi nchini Poland na Bulgaria wakati mzozo nchini Ukraine ukiendelea kutokota. Andriy Yermak, mkuu wa utumishi katika ofisi ya Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema Urusi inajaribu kuuvunja umoja wa washirika wa Ukriane kwa kutumia raslimali za nishati kama silaha. Kampuni ya gesi ya Poland inayomilikiwa na serikali PGNiG imesema usambazaji wa gesi kutoka kampuni kubwa ya nishati ya Gazprom kupitia Ukraine na Belarus unasitishwa leo asubuhi. Warsaw imesema wateja wake hawapaswi kuwa na wasiwasi kwa sababu hifadhi yake ya gesi kwa sasa ni asilimia 76. Waziri wa nishati wa Bulgaria amesema Gazprom iliitumia kampuni ya Bulgargaz ujumbe kama huo. Poland imekataa kulipia gesi yake katika sarafu ya Kirusi ya rouble, kama inavyotaka Urusi ili kuongeza thamani ya sarafu yake kutokana na vikwazo vya nchi za Magharibi. Poland inaiunga mkono Ukraine na imeikaribisha idadi kubwa kabisa ya wakimbizi wa Ukraine kuliko nchi nyingine yoyote.