Wajumbe kutoka nchi 40 wanakutana kwa ajili ya kikao cha dharura kwenye mji wa Ramstein wa nchini Ujerumani kujadili njia za kuimarisha ulinzi wa Ukraine. Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin, mawaziri wa ulinzi na maafisa wakuu wa kijeshi kutoka duniani kote wanakutana kwenye kikao hicho kinachoongozwa na waziri wa ulinzi wa Marekani. Kikao hicho kinafanyika kwenye kituo cha jeshi la anga la Marekani kilichopo kusini magharibi mwa Ujerumani. Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin anaamini kuwa Ukraine inaweza kushinda vita dhidi ya Urusi ikiwa itapatiwa nyenzo muhimu zinazohitajik. Wajumbe kwenye mkutano huo wanajadili njia za kuipatia Ukraine silaha ili iweze kujihami dhidi ya Urusi kwenye sehemu ya mashariki ya nchi hiyo. Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov ameonya juu ya hatari ya kutokea vita vikuu vya tatu na amesema hatari ya kutokea vita hivyo imekuwa kubwa.