Ibenge apata ajali Morocco

Kocha Mkuu wa RS Berkane, Florent Ibenge amepata ajali ya gari wakati akitoka mazoezini jana.

Taarifa ya klabu yake imesema ajali hiyo imempa maumivu makali ya mgongo kocha huyo Mkongomani.

Vipimo vilivyofanywa kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Mohammed VI vimeonyesha kocha huyo ameumia katika eneo hilo na atalazimika kupumzishwa kwa muda wa wiki moja mpaka siku 10.

Ajali hiyo imekuja ikiwa ni siku moja tangu Ibenge aiwezeshe Berkane kucheza nusu fainali ya tatu katika mashindano ya Afrika katika kipindi cha miaka minne.

Berkane imetinga hatua hiyo baada ya juzi kuitupa nje Al Masry ya Misri kwa faida ya bao la ugenini kufuatia kufungwa mabao 2-1 nchini Misri kisha na wao kushinda bao 1-0 na kufanya matokeo ya jumla kuwa 2-2.

Berkane sasa itakabiliana na TP Mazembe ya DR Congo katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho wakianzia jijini Lubumbashi kisha timu hizo kumalizana nchini Morocco.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii