Kichuya azungumzia ishu yake na Yanga

Rekodi zinaonyesha namna winga wa Namungo FC, Shiza Kichuya anavyokuwa tishio kwa Yanga, wakikutana mechi za Ligi Kuu Bara.

Kichuya amekuwa mwiba kwa Yanga tangu akiwa na Simba, hivyo anachokifanya akiwa na Namungo FC ni muendelezo wa alichokifanya nyuma.

Kichuya akiwa Simba baadhi ya mechi alizoifunga Yanga ni msimu wa 2016/17 mzunguko wa kwanza alitoa asisti ya bao la kwanza lililofungwa na Mavugo, huku akifunga la pili, timu yake ikishinda 2-1.

2017 Kichuya alifunga bao la kideo alichonga mpira wa kona, ulikwenda moja kwa moja nyavuni na dakika 90 zilimalizika kwa sare ya bao 1-1 ( bao la Yanga lilifungwa na Tambwe).

Kama haitoshi mwaka 2018 Kichuya alitoa asisti ya bao alilofungwa Erasto Nyoni, Simba ikiibuka na ushindi wa bao 1-0.

Kichuya kuifunga Yanga akiwa na Namungo FC, mechi ya Aprili 23 timu yake ikichapwa mabao 2-1 ni muendelezo wa rekodi zake za nyuma.

“Ninamiliki mabao matatu kwenye ligi, nimezifunga timu tofauti, hivyo mashabiki waache kunilisha maneno kwamba naikamia Yanga, kama haitoshi Mayele aliweka dhamira ya kutufunga katufunga,”alisema Kichuya na kuongeza;.

“Kabla ya mechi kocha aliniambia nifunge bao kwa ajili yake, nimetimiza ahadi yake, pia kuifunga Simba, Yanga na Azam FC mchezaji unajisikia kiwango chako kipo juu.”

Alisema kuifunga Yanga ni kutimiza majukumu yake kama ilivyo kwa wachezaji wengine, huku akisisitiza kutamani kufunga kila anapopata nafasi.

“Hata Mayele kuna mechi anafunga mzunguko wa kwanza na wa pili,alifanya hivyo na Azam FC, pia kuna mechi hafungi, ndiyo maana nasema kazi yangu ni kucheza ikitokea nimefunga ndivyo hivyo,”alisema.

Ukiachana na Kichuya, straika wa timu hiyo, Reliant Lusajo alisema anaamini bado ataendeleza mchakamchaka wa kuwania kiatu cha dhahabu.

“Kama sijaifunga Yanga nitafunga mechi nyingi zilizopo mbele tetu, kwa sasa nina mabao 10 ila yataongezeka tu, kwani mechi bado ni nyingi.” alisema.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii