Mfalme wa Abdullah wa Jordan amekubaliana na Rais wa Marekani Joe Biden kuhusu haja ya kuzuia marudio ya makabiliano ya karibuni katika maeneo matakatifu ya Kiislamu mjini Jerusalem ambayo yalisababisha wasiwasi wa kuzuka vita. Katika mazungumzo ya simu jana, Abdullah alinukuliwa akisema kuwa msingi wa amani ni makubaliano kati ya Waarabu na Israel ya suluhusho la mataifa mawili ambapo taifa la Palestina litaundwa jirani na Israel. Abdullah ambaye ukoo wake ndio mtunzaji wa maeneo ya kiislamu na Kikristo katika Mji wa Kale, ameongoza juhudi za kidiplomasia kuiwekea mbinyo Israel, ambayo anailaumu kwa kuongezeka kwa mvutano katika eneo la msikiti wa al-Aqsa, linalofahamika kwa Wakristo kama Temple Mount. Wakati huo huo, Israel imesema itakifungua tena kivuko chake pekee kutoka Gaza kwa ajili ya wafanyakazi ikiwa ni siku mbili baada ya kukifunga. Ni baada ya kuwa na utulivu wa mashambulizi ya maroketi kutoka Ukanda huo wa Wapalestina. Kivuko hicho hutumiwa na Wapalestina 12,000 walio na vibali vya kuingia Israel kufanya kazi.