WATANZANIA WALIOKO MAREKANI WADAI KATIBA MPYA

Madai ya Katiba mpya yameibukia nje ya viunga vya Ubalozi wa Tanzania Jijini New York, Marekani, ndivyo unavyoweza kusema.

Hiyo ni baada ya waandamanaji kujitokeza nje ya ofisi ya ubalozi jana wakiwa wamebeba mabango yenye ujumbe tofauti waliolenga kuufikisha kwa Rais Samia Suluhu Hassan aliyeko nchini humo.

Waandamanaji hao waliokuwa wakiimba “Katiba mpya ni sasa”, walikuwa wamenyanyua juu mabango yaliyokuwa yameandikwa pia ujumbe uliosomeka tunataka uraia pacha.

Hata hivyo, baadaye Rais Samia alizungumzia hoja zao wakati akizungumza na Watanzania waishio nchini humo, alisema “uzuri wenyewe wakati nakuja hapa, nimewakuta wanangu hapa wamejipanga na mabango na fulana zao nikawaambia nimewaona. Lakini ni haki yao waseme tuwasikie.

“Nimesoma mabango yao na fulana zao na ujumbe wao, ila niseme tu, kwa hali ya kisiasa tupo vizuri na mambo yote haya yako katika task force (kikosi kazi) yanazungumzwa na wenyewe watatuletea,” alisema Rais Samia.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii