WAKALA
wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini(RUWASA)Wilaya ya Nachingwea
mkoani Lindi umesema kupatikana kwa miradi ya maji inayotekelezwa kwa
fedha za UVIKO-19 ambazo zimetolewa na Serikali ya Awamu ya Sita
itakwenda kuongeza kiwango cha upatikanaji maji ndani ya wilaya hiyo.
Akizungumza
na waandishi wa habari, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Nachingwea Sultan
Ndoliwa amesema Wilaya hiyo kwa sasa inaendelea na utekelezaji wa miradi
ya maji mitano ukiwemo mradi wa maji Mchangani ambao unatekelezwa kwa
fedha za UVIKO-19.
“Hapa tuko kwenye Kijiji cha Mchangani na
mradi huu wa maji ambao tunaotekeleza unagharimu sh.milioni 475 na
utakuwa na vituo vinane vya kuchotea maji na una mtandao wa bomba
kilometa 14.5.Mradi huu unakwenda kunufaisha watu 3,682
utakapokamilika,”amesema.
“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan
kwa kutoa fedha ili kufanikisha miradi hii kwa lengo la kuondoa
changamoto ya upatikanaji maji maeneo ya vijijini, kwetu tunasema miradi
hii inayotekelezwa kwa fedha za UVIKO-19 imekuja wakati muafaka, kwani
tunakwenda kutatua changamoto ya uhaba wa maji kwa wananchi wa Wilaya
yetu ya Nachingwea.”
Aidha amesema mradi mwingine
wanaoutekeleza kwa fedha za ustawi ni mradi wa maji katika kijiji cha
Lionjo unaogharimu fedha Sh.milioni 309 na utakapokamilika utahudumia
watu 3546 , kwa sasa uko hatua za awali na utakuwa na vituo tisa vya
kuchotea maji.
“Mradi mwingine ambao RUWASA Wilaya ya Nachingwea
tunautekeleza ni mradi wa maji katika Kijiji cha
Ruponda,Namanga,Mwanyamala na Nyangawa ambao unagharimu Sh.milioni 761
na utakapokamilika utahudumia watu watu 6220.
Mhandisi Ndoliwa
amesema kwa ujumla miradi hiyo ya maji ikiwemo inayotekelezwa kwa fedha
za UVIKO-19 ikikamilika itaongeza upatikanaji wa maji kutoka asilimia ya
sasa 62 hadi asilimia 73 na jumla ya fedha zote zinazotekeleza miradi
ni Sh.bilioni 1.6.
Kuhusu kufukia asilimia 85 ya upatikanaji wa
maji ifikapo mwaka 2025, amesema baada ya kukamilisha miradi hiyo pamoja
na miradi mingine minne ambayo wanatarajia kuanza kuitekeleza
watafikia asilimia hiyo.
Alipoulizwa kuhusu vyanzo vya maji
vilivyopo kwenye Wilaya hiyo, amesema wanategemea visima virefu lakini
pia kuna vyanzo vya maji ya chemchem kupitia bomba ku.
Kwa
upande wake Mhandisi Milembe Lukenza ambaye ni Msimamizi wa mradi wa
maji Mchangani unaotekelezwa kwa fedha za UVIKO-19 amesema kuwa
anamshukuru Rais Samia kwa kuonesha upendo wake kwa wananchi wa wilaya
ya Nachingwea kwa kuamua kuwapelekea mradi huo wa maji.
Ametumia
nafasi hiyo kutoa rai ka wakandarasi wanawake wote ambao wamekuwa
sehemu ya kusimamia miradi ya maji inayotokana na fedha hizo wahakikishe
wanatekeleza majukumu yao kwa weledi, ufanisi na uaminifu mkubwa na
kwamba wanawake wanayo nafasi ya kushiriki kikamilifu katika kuleta
maendeleo ya Taifa la Tanzania.
Awali Mhandisi wa Mkandarasi wa
Kampuni ya Kharton Traders Limited Daud Omari ambaye ni Msimamizi wa
ujenzi wa tanki lenye ujazo wa lita 100,000 katika mradi huo amesema
wanamshukuru Rais Samia kwa kuwakumbuka wakandarasi wazawa katika
kujenga miradi hiyo ya maji.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi
wa wa Kijiji cha Mchangani wamesema wanatoa shukrani kwa RUWASA pamoja
na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia kwa kuamua
kutatua changamoto ya maji katika kijiji hicho.
“Tunamshukuru
Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea mradi huu wa maji wilayani
Nachingwea na hasa katika Kijiji cha Mchangani , kupata mradi huu maana
yake ni moja tu tunakwenda kuondokana na adha ya kufuata maji umbali
mrefu, hata wanafunzi watakuwa wanawahi shule kwani watakuwa wakichota
maji karibu tofauti na ilivyo sasa.”