Mkoa wa manyara unalenga kuwachanja
watoto wenye umri wa chini ya miaka 5 kuwakinga dhidi ya ugonjwa wa
Polio unaosababisha kupooza.
Kampeni hiyo itakayozinduliwa rasmi
kuanzia April 28 na kukamilika Mei Mosi mwaka huu inalenga kuwachanja na
kuwalinda watoto zaidi ya laki tatu wa umri wa chini ya miaka mitano
dhidi ya ulemavu na vifo kutokana na mlipuko wa polio ulioibuka nchi
jirani ya Malawi.
Kwa mujibu wa Mganga mkuu mkoa wa Manyara Damas
Kayera Mpango huo wa dharura wa chanjo utafanyika kwa kuwekwa matone ya
chanjo kwenye midomo ya watoto mkoani kote nyumba hadi nyumba na katika
shule za msingi.
Kayera amewaambia waandishi wa habari kuwa
watawafikia watoto kwa asilimia 100%, lengo likiwa kuwaweka watoto wote
mkoani humo salama.
"Tumelenga kuwafikia watoto 351, 364 walio
chini ya miaka mitano na hii ni kuhakikisha kwamba wanazuiwa na ugonjwa
huu wa Polio ambao umeonekana kuanza kule Malawi, hivyo tunataka huu
ugonjwa hapa mkoani kwetu usiwepo hivyo tunahitaji wananchi wetu wawe na
afya bora ili waweze kujiletea maendeleo yao". Amesema Dkt Kayera.
Mtaalamu
wa Epidemiolojia kutoka Wizara ya Afya Dokta Witness Mchwampaka amesema
wamejipanga kuzifikia jamii za kifugaji na wawindaji wa Kihadzabe
katika kufanikisha chanjo hiyo.
"Tutafika maeneo yote hadi kwa
Wahadzabe na huko tutakutana na wale watu ambayo wanaushawishi mfano kwa
jamii zile za kimaasai tutawatumia malaigwanani wanaweza kutusaidia
zoezi hili kuwa jepesi zaidi". Amesema Dkt Mchwampaka
Kwa upande
wake mratibu wa chanjo mkoa wa Manyara Suleiman Manoza amesema kwa kila
halmashauri wametenga timu maalumu kutumia pikipiki kufikia maeneo
magumu kufikika.
" Tumejipanga vizuri na tumepanga timu maalaumu
ambayo itakuwa na usafiri wa pikipiki ambayo inauwezo wa kufika mahala
popote na maeneo yote yatafikiwa". Amesema Manoza.