Gari la Rais Samia la Royal Tour lavutia utalii

Baada ya filamu ya Royal Tour kuzinduliwa katika miji ya New York na Los Angeles Marekani, gari lililoonekana likiendeshwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika filamu hiyo, limekuwa kivutio kipya cha utalii katika Hifadhi ya Serengeti.

Gari hilo aina ya Toyota Land Cruiser Hardtop lililoongezwa ukubwa kwa ajili ya shughuli za kitalii, Samia alionekana akiliendesha akiwa na mtayarishaji wa filamu hiyo, Peter Greenberg.

Kwa mujibu wa tovuti ya Toyota, aina hiyo ya gari kwa sasa inauzwa Sh198.9 milioni.

Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) imeliarifu Mwananchi kuwa, baada ya uzinduzi wa filamu hiyo watalii wa ndani na nje waliotembelea hifadhi ya Serengeti wamehamasika kuliona.

“Baada ya uzinduzi wa filamu watalii wengi wa ndani na nje ambao wamepata bahati ya kuliona gari hili ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti wamekuwa na hamasa na msisimko mkubwa kuliona gari hilo lililotumiwa na Rais kwenye filamu ya Royal Tour,” ilieleza taarifa ya Tanapa.

Mbali na Samia, Tanapa ilisema gari hilo limewahi kutumiwa na viongozi mbalimbali walipotembelea hifadhi hiyo, akiwemo Rais Mstaafu wa awamu ya nne Jakaya Kikwete. “Maandalizi yalihusisha marekebisho ya friji ili kufanya kuwa na vinywaji baridi, maboresho ya siti na kuweka red carpet ili kuwa na muonekano wa ki VIP, kuongeza nafasi na kulinganisha na mazingira na alilichagua Rais mwenyewe,” ilieleza taarifa hiyo.

Filamu hiyo yenye urefu wa saa moja na dakika 58 inauzwa kwa dola 19.99 za Marekani (sawa na Sh46,476) na inakodishwa kwa dola 5.99 za Marekani (sawa na Sh13,926) katika mtandao huo.

Kupitia ukurasa wake wa twitter, Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, Tundu Lissu alihoji iwapo Serikali inapata chochote katika mauzo hayo kwa kuwa Royal Tour ni biashara kubwa Amazon.

Alipoulizwa kwa njia ya WhatsApp kuhusu hilo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana akiwa nchini Marekani alielekeza maswali hayo aulizwe Katibu Mkuu, Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Hassan Abbas ambaye alipopigiwa simu yake ya kiganjani iliita bila kupokelewa.

Filamu hiyo hadi kukamilika, imegharimu Sh bilioni saba, kati ya Sh11 bilioni zilizochangishwa kutoka mashirika mbalimbali.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii