Uturuki yafunga anga lake kwa ndege za Urusi kuelekea Syria

Uturuki imefunga anga lake kwa ndege za kiraia na kijeshi za Urusi zinazosafiri kuelekea Syria.Tangazo hilo linaashiria moja ya majibu makali zaidi ya Uturuki, ambayo imejenga uhusiano wa karibu na Moscow licha ya kuwa mwanachama wa jumuiaya ya kujihami ya NATO, kutokana na mashambulizi ya kijeshi ya Urusi nchini Ukraine katika kipindi cha miezi miwili. Vyombo vya habari vya Uturuki vimemnukuu waziri wa mambo ya nje Mevlut Cavusoglu, akisema kuwa uamuzi huo aliuwasilisha kwa mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov, na baada ya siku mbili Rais Vladimir Putin wa Urusi alitoa amri ya kutotumia anga hilo. Uturuki imesema marufuku hiyo itadumu kwa kipindi cha miezi mitatu. Hata hivyo hakukuwa na majibu ya mara moja kutokana na tangazo hilo kutoka kwa Urusi ambayo pamoja na Iran zimekuwa waungaji mkono muhimu wa rais wa Syria Bashar al-Assad wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya nchi hiyo iliyoharibiwa vibaya. Uturuki imekuwa ikijaribu kusuluhisha mzozo huo, ikiandaa mikutano ya wajumbe wa majadiliano wa Urusi na Ukraine mjini Istanbul, na mwingine kati ya Lavrov na mwenzake wa Ukraine Dmytro Kuleba mjini Antalya.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii