Mamiliaoni ya watu nchini Somalia wako hatarini kutumbukia kwenye baa la njaa ambapo watoto ndio hasa wanaokabiliwa na hatari hiyo inayotokana na ukame ulioongezeka nchini humo. Tahadhari hiyo imetolewa leo na Umoja wa Mataifa. Taarifa ya mashirika ya Umoja huo wa mataifa imesema wasomali asilimia 40 wanakabiliwa na mazingira ya njaa kutokana na ukosefu wa mvua,ongezeko kubwa la bei ya vyakula pamoja na kukosekana msaada wa fedha. Maeneo mengi ya nchi hiyo ya upembe wa Afrika yanakumbwa na ukame ambao pia umeziathiri nchi nyingine katika ukanda huo zikiwemo Ethiopia na Kenya,ingawa mashirika ya Umoja wa Mataifa yametoa tahadhari kwamba msaada mkubwa fedha unakosekana katika kushughulikia mgogoro huo ili kuepusha marudio ya baa la njaa lililoshuhudiwa mnamo mwaka 2011. Mashirika ya Umoja wa Mataifa yaliyotoa tamko hilo ni lile la mpango wa chakula duniani WFP,la chakula na kilimo,FAO,pamoja na la msaada wa kibinadamu OCHA na lile la mfuko wa kusaidia watoto Unicef.