Mamlaka nchini Ukraine zimesema huenda maelfu ya watu wameuawa
kufuatia mashambulizi ya Urusi katika mji wa bandari wa Mariupol, na
kuishtumu Urusi kuchelewesha kimakusudi zoezi la kuhamisha watu kutoka
mji huo uliozingirwa, ambao unatajwa kuwa uko hali mbaya. Katika ujumbe
wake kwa njia ya video kwa bunge la Korea Kusini, Rais wa Ukraine
Volodymyr Zelenksiy amesema mji wa Mariupol umeharibiwa, na kwamba
maelfu ya watu wamekufa lakini licha ya hayo, Urusi bado inaendeleza
mashambulizi yake. "Katika maeneo yaliyochukuliwa na Urusi, jeshi la
nchi hiyo kwa makusudi limewalenga waalimu, watu wanaohusika na jeshi la
Ukraine na utendaji wa serikali, wanaharakati, waandishi habari. Watu
ambao wanaelimisha jamii na kutetea umoja wa kitaifa. Watu wa aina hiyo
walitekwa nyara, waliuawa kwa makusudi. Hiyo ilikuwa ni amri, ilikuwa ni
mbinu."Shirika la habari la Reuters limethibisha uharibifu mkubwa
katika mji huo lakini halikuweza kuthibitisha idadi kamili ya watu
waliokufa katika mji huo wa kimkakati, ulioko kati ya Crimea
inayodhibitiwa na Urusi na maeneo ya mashariki mwa Ukraine
yanayoshikiliwa na wapiganaji wanaotaka kujitenga na ambao wanaungwa
mkono na Urusi.