Benki ya Dunia imesema kuwa uchumi wa Ukraine unatarajiwa kudorora kwa karibu nusu kutokana na uvamizi wa Urusi kufunga biashara na kupunguza mauzo ya nje.Katika ripoti yake iliyoitoa jana Jumapili, Benki ya dunia imesema uchumi wa Ukraine huenda ukapungua kwa asilimia 45.1 mwaka huu, huku pato la taifa la Urusi likitarajiwa kushuka kwa asilimia 11.2. Makamu wa rais wa Benki ya Dunia kanda ya Ulaya na Asia Anna Bjerde, amesema mauzo ya ngano ya Ukraine na shughuli nyingine za kiuchumi vimetatizika katika maeneo mengi ya nchi kutokana na miundombinu kuharibiwa. Wataalamu wa uchumi wanatabiri kuwa pato la taifa katika kanda ya Ulaya Mashariki, inayojumuisha nchi za Ukraine, Belarus na Moldova, litaporomoka kwa asilimia 30.7 mwaka huu, kutokana na vita hiyo.