Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anaongoza katika duru ya kwanza ya uchaguzi uliofanyika jana Jumapili akifuatiwa na mpinzani wake wa karibu Marine Le Pen mwenye siasa kali za mrengo wa kulia. Wizara ya mambo ya ndani ya Ufaransa imesema kwamba kulingana na matokeo ya awali, Macron anaongoza kwa asilimia 27.6 dhidi ya asilimia 23.0 alizopata Le Pen. Wanasiasa hao wawili sasa wanatarajiwa kuchuana katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais utakaofanyika Aprili 24. Duru ya pili inatarajiwa kuwa na ushindani mkali kati ya Macron, mwanasiasa anayepigia upatu Umoja wa Ulaya na Le Pen mwenye siasa za mrengo mkali wa kulia. Utafiti wa kura za maoni umetabiri kuwa Macron huenda akaibuka na asilimia 54 ya kura katika duru ya pili ya uchaguzi.