Kufuatia kuvunjwa vioo vya madirisha ya madarasa 12 katika shule ya Sekondari Kibedya iliyopo wilayani Gairo mkoani Morogoro, uongozi wa wilaya hiyo umemsimamisha kazi mkuu wa shule hiyo Kelvin Kayombo ili kupisha uchunguzi.
Madarasa hayo yamejengwa kwa fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19 maarufu kama madarasa ya mama Samia, kwa gharama ya Sh120 milioni ambazo zilipokelewa kwa ajili ya ujenzi huo wa madarasa.
Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Jabir Makame alisema hayo leo Jumapili Aprili 10, 2022 wakati akizungumza na Mwananchi ambapo ameeleza kuwa alifika katika shule hiyo baada ya kupata taarifa ya kutokea kwa tukio hilo.
Makame amesema amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo kumsimamisha kazi mkuu huyo wa shule, ili kupisha uchunguzi pamoja na kuchukua hatua zingine ikiwamo kukamatwa kwa watu watatu wanaotuhumiwa kuhusika na tukio hilo akiwamo mlinzi wa shule hiyo.
“Mlinzi wa shule hiyo tumemuhoji mbele ya kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya, amekiri siku ya tukio hakuwepo eneo lake la kazi, kilichonishangaza shule imefungwa miundo mbinu ya umeme, ila siku ya tukio umeme hakuwepo, kumbe luku imeisha muda mrefu na uongozi wa shule haukuhangaika kununua, hii ni hatari,”amesema mkuu huyo wa wilaya.
Amesema licha ya kukamatwa kwa watu watatu na kusimamishwa kazi kwa mkuu wa shule, Mkuu huyo wa wilaya ameagiza watu wote waliohusika na uharibifu huo kulipa gharama za kuweka upya vioo vilivyovunjika, wakati mashauri yao yakiendelea kwenye vyombo vya sheria.
Makame amewataka wananchi kila mmoja kutambua wajibu wake wa kuwa mlinzi wa mali za umma na kwamba tukio hilo limeleta fedheha ikizingatiwa wilaya ya Gairo pekee ilipokea Sh1.1 bilioni kutoka mpango huo wa Uviko-19 kwaajili ya ujenzi wa madarasa.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Gairo, Shaban Sajilo amelaani kitendo hicho huku akipongeza hatua ambazo zinaendelea kuchukuliwa dhidi ya wahusika.
“Niiombe kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya, kuendela kuchukua hatua, nimesikia mlinzi amekamatwa yuko ndani, lakini ufanyike msako wa uhakika, na mtu huyu akishakamatwa tuone asilimia 100 ya sheria inafuata mkondo wake, kusiwepo na huruma hata kidogo,”alisema
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Kibedya, Butindi Masatu amebainisha kuwa wahusika wote waliofanywa tukio hilo wanatakiwa kusakwa na kuwajibishwa kwa mujibu wa sharia.
Inadaiwa sababu ya kuvunjwa vioo hivyo ni wivu wa kimapenzi ambapo mtuhumiwa alimtuhumu mlinzi kuwa na mahusiano na mkewe, hoja ambayo licha ya kutajwa na viongozi na wanakijiji, imeshindwa kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Fortunatus Musilim kutokana na kuahidi kulifanyaia na kulitolea taarifa.
Baadhi ya Wananchi wa Gairo waliozungumza na Mwananchi wamelaani kitendo hicho wakisema kuwa hata kama kulikuwa na ugomvi binafsi, haukupaswa kuhusishwa na mali za umma, kwani madarasa hayo yanalenga kusaidi, kuinua na kuboresha kiwango cha elimu kwa wananchi wote bila ubaguzi.