Morocco na Uhispania wakubaliana kumaliza mvutano wa kidiplomasia

Morocco na Uhispania zimekubaliana kufungua ukurasa mpya wa mahusiano baada ya serikali mjini Madrid kutangaza kuunga mkono ajenda ya Morocco ya kulidhibiti jimbo linalozozaniwa la Sahara Magharibi. Katika mkutano mjini Rabat kati ya waziri mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez na mfalme Mohammed wa VI wa Morocco viongozi hao wawili wameafikiana kumaliza mzozo wa kidiplomasia wa karibu mwaka mmoja kwa kufanya kazi chini ya misingi ya kushirikiana na kuheshimiana. Waziri Mkuu Sanchez pia alirejea msimamo wa serikali yake uliotolewa mwezi uliopita akisema mpango wa Morocco kuhusu kulipatia jimbo la Sahara Magharibi uhuru wa ndani ni msingi madhubuti katika kutatua mzozo uliopo. Hata hivyo, mpango huo unapingwa vikali na vuguvugu la Polisario la Sahara Magharibi linaloungwa mkono na taifa jirani la Algeria na pande hizo mbili zinataka kuitishwe kura ya maoni kuhusu wa jimbo hilo.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii