Faharasa mpya iliyochapishwa leo imeonesha kuwa bei ya vyakula duniani imepanda na kufikia rekodi ya juu kabisa mnamo mwezi Machi baada ya vita nchini Ukraine kusababisha mtikisiko mkubwa kwenye masoko ya nafaka na mafuta ya kupikia. Katika ripoti hiyo inayotolewa na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani, FAO bei za vyakula zimepanda kwa alama 159.3 kwa mwezi Machi ikilinganishwa na alama 140 za mwezi Februari kiwango ambacho tayari kilivunja rikodi. Urusi na Ukraine ni wasafirishaji wakubwa wa ngano, mahindi, shayiri na mafuta ya alizeti kupitia Bahari Nyeusi, lakini vita vya wiki sita kwenye kanda hiyo vimetatiza usafirishaji wa mazao na bidhaa nyingi kutoka Ukraine. Shirika la FAO limeonya kuwa bei za vyakula huenda zitapanda kwa asilimia 20 na kuongeza kitisho cha kupanda kiwango cha utapiamlo katika wakati hatma ya vita kati ya Urusi na Ukraine bado haijulikani.