Muda mfupi baada ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, Innocent Bashungwa kutoa maagizo kwa uongozi wa Jiji la Mwanza kutokana na video iliyosambaa mtandaoni ikionyesha watu wanaodaiwa kuwa mgambo wakirusha bidhaa ikiwamo matunda ya mmachinga aliyekuwa akizunguka mtaani kutafuta wateja, Mkuu wa Mkoa huo (RC), Robert Gabriel amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana (DC), Amina Makilagi kuwaondolea hadhi ya kuwa askari wa jeshi la akiba mgambo wote waliohusika katika tukio hilo huku akimsimamisha kazi mratibu wa upangaji wa machinga wa Jiji hilo.
Jana Jumamosi Aprili 16, 2022 Waziri Bashungwa alitoa maagizo akiwawataka wakurugenzi na wakuu wa wilaya za Mkoa huo kujitathmini iwapo wanastahili kuendelea kuwepo kwenye nafasi zao akimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel kufuatilia wahusika wa tukio hilo na hatua kali zichukuliwe dhidi yao.
Waziri huyo wa Tamisemi alitoa maagizo kupitia akaunti yake ya rasmi ya Instagram akisema; "Nimeona video inayosambaa mtandaoni ikionyesha matunda aina ya ndizi ya mfanyabiashara mdogo yakipakiwa na mgambo kwenye gari aina ya Toyota Hilux. Inasemekana tukio hili limetokea jijini Mwanza. Nimemuagiza Mkuu wa Mkoa, Gabriel Luhumbi kufuatilia kubainisha wahusika na hatua kali zichukuliwe dhidi yao,"
"Ninaendelea kuwaelekeza wakuu wa mikoa kote nchini kuhakikisha zoezi la kuwapanga wafanyabiashara wadogo wamachinga linafanyika kwa utulivu na amani na kujali utu. Wakurugenzi na wakuu wa wilaya mpaka haya yanatokea kwenye maeneo yenu mjitathmini kama mnatosha," alisema Bashungwa
Muda mfupi baada ya Waziri huyo kutoa maagizo, RC Gabriel alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana (DC), Amina Makilagi kuwachukulia hatua mgambo saba wanaodaiwa kuhusika na tukio hilo pamoja na kumsimamisha kazi mratibu wa Jiji la Mwanza wa upangaji wa wafanyabiashara ndogondogo maarufu machinga kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake
RC Gabriel amesema “Namuagiza Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana kuwaondolea hadhi ya kuwa askari wa jeshi la akiba kikosi chote kilichohusika katika tukio hilo mara moja kuanzia muda huu ikiwa na maana kwamba hawataweza kufanya kazi tena kama jeshi la akiba”
“Pili namsimamisha majukumu yake mratibu wa Jiji la Mwanza wa zoezi la upangaji wa machinga kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake”
Pia, Mkuu huyo wa Mkoa amelaani vikali kitendo hicho cha mgambo kuwasumbua wafanyabiashara hao.