Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson ataitembelea India katikati ya wiki inayokuja kwa mazungumzo juu ya biashara na usalama pamoja mwenzake, Narendra Modi, ambaye amejizuia kuilaani Urusi kutokana na vita vinavyoendelea nchini Ukraine. Katika taarifa yake kuelekea ziara hiyo itakayokuwa ya kwanza akiwa kiongozi wa Uingereza, Johnson amesema ni muhimu kwa washirika na mataifa ya kidemokrasia kusimama pamoja katika wakati ambapo amani na ustawi vinahujumiwa na madola ya kiimla. Uingereza, ambayo imejiunga na mataifa mengine ya Magharibi kuiwekea vikwazo Urusi kutokana na vita vya Ukraine, inatofautiana na India iliyojizuia kuilaani Moscow hadharani au kupiga kura kukosoa uamuzi wa Kremlin wa kutuma jeshi lake nchini Ukraine. Ingawa Johnson amesema mazungumzo na Modi yatatuama juu ya kuimarisha ushirikiano kati ya madola hayo mawili, suala la Ukraine linatarajiwa pia kuwa ajenda kuu.