Serikali ya Tanzania na Umoja wa Falme
za Kiarabu (U.A.E), zimesaini Makubaliano ya Tume ya Kudumu ya Pamoja
katika nyanja za forodha, elimu, kilimo, nishati, mawasiliano, ulinzi na
usalama.
Makubaliano hayo yamesainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula na Waziri
wa Nchi wa UAE, Shakhbout bin Nahyan Al Nahyan katika Mkutano wa Tume ya
Kudumu ya Pamoja kati ya Tanzania na UAE leo Jijini Dar es Salaam
Akizungumza
katika hafla hiyo iliyotanguliwa na kikao cha Makatibu Wakuu, Waziri
Mulamula amesema kusainiwa kwa makubaliano hayo ni ishara tosha ya
kunaimarika zaidi kwa ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili.
“Kusainiwa
kwa makubaliano hayo kunatoa fursa kati ya Serikali ya Tanzania na
Umoja wa Falme za Kiarabu kuendeleza biashara na uwekezaji ,” amesema
Balozi Mulamula
Kwa upande wake Waziri wa nchi wa UAE Mhe.
Sheikh Shakhboot Nahyan Al Nahyan amesema ni faraja kwa kwa kusainiwa
kwa makubaliano hayo kwani wamesubiri kwa muda, na kilicho bakia ni
utekelezaji wa maeneo waliyokubaliana kwa maslahi ya mataifa yote.
“Natumaini
yale tuliyozielekeza chemba za biashara za pande zote mbili kuhakikisha
kuwa zinashirikiana zaidi katika kuboresha zaidi mazingira ya bishara
na uwekezaji kwa maslahi ya pande zote mbili,” amesema Mhe. Al Nahyan
“Baada
ya kusainiwa kwa makubaliano haya tumedhamiria kuanza kuongeza maeneo
ya ushirikiano baina yetu katika sekta za elimu, nishati, kilimo,
biashara na mawasiliano,”amesema Al Nahyan.
Awali, akiwasilisha
hotuba yeke, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab amesema kusainiwa kwa makubaliano
ya Tume ya Kudumu ya pamoja kati ya Tanzania na UAE ni wazi kuwa
ushirikiano baina ya Tanzania na UAE utazidi kuimarika zaidi.
“Pamoja
na mambo mengine, kikao cha Makatibu Wakuu tumejadili na kukubaliana
kuongeza ushirikiano katika nyanja za biashara na uwekezaji,
mawasiliano, usafirishaji pamoja na ulinzi na usalama……kusainiwa kwa
makubaliano haya kunaakisi ishara nzuri ya kuendeleza ushirikiano baina
yetu,” amesema Balozi Fatma
Naye Balozi wa Tanzania katika Umoja
wa Nchi za Falme za Kiarabu (UAE) Balozi Mohammed Mtonga amebainisha
fursa mbalimbali zinazopatika katika Falme za Kiarabu ikiwa ni pamoja na
masoko ya matunda, nyama na korosho.
Mkutano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja kati ya Tanzania na UAE ulifanyika mwaka 2016.