SERIKALI ya Uingereza kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi hiyo Priti Patel inataraji kusaini mkataba na serikali ya Rwanda ambao utadumu kwa muda wa miaka mitano 5 wenye dhumuni la serikali ya Rwanda kupokea wakimbizi haramu wanaoingia nchini Uingereza.
Mkataba huo utaigharimu serikali ya Uingereza Zaidi ya paundi milioni 120 kwa kila mwaka ambayo itazilipa kwa serikali ya Rwanda ikiwa kama sehemu ya gharama zitakazotumika kuwahudumia wakimbizi hao haramu.
Mpango wa serikali ya Uingereza ni kupunguza au kuzuia kabisa uingiaji wa wahamiaji haramu ambao namba yao imeongezeka kufikia watu 28,500 kwa mwaka.
Katika hotiba yake Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson amesema:
“Hatuwezi kuendelea kuvumilia mfumo huu wa uingiaji wa wahamiaji haramu, sawa tuna nia njema lakini uwezo wetu wa kuwasaidia watu hauruhusu.”
Kwa upande mwingine mpango huo unataraji kukosolewa vikali na mashirika ya kutetea haki za binadamu pamoja na wanasiasa wa vyama vya upinzani nchini Uingereza kutokana na kile kinachoonekana kuwa ni ukiukwaji wa haki za binadamu.
Yvette Cooper Katibu Mkuu Kivuli wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uingereza ameliambia Gazeti la The Guardian kuwa ni tangazo la aibu lililokuwa na lengo la kuficha uvunjifu wa sheria uliofanywa na Waziri Mkuu Boris Johnson.
Cooper ametoa sababu akisema mpango huo hautekelezeki, hauna maadili na ni wa kinyonyaji ambao utawagharimu walipa kodi wa Uingereza mabilioni ya pesa hasa katika wakati huu ambao kuna janga la ugumu wa maisha na itawia vigumu kwasababu si rahisi kupata maamuzi sawia kutoka kwa wahamiaji wenyewe.