Shirika la fedha ulimwenguni IMF limeidhinisha kuundwa kwa mfuko mpya
wa ufadhaili unaolenga kuzisaidia nchi za kipato cha chini na za kati
kukabiliana na changamoto za muda mrefu ikiwemo mabadiliko ya tabia nchi
na milipuko ya majanga. Mkuregenzi mtendaji wa IMF Kristalina Georgieva
ametangaza uidhinishwaji wa mfuko wa ustahimilivu utakaonza kutumika
mwanzoni mwa mwezi Mei, ukilenga kukusanya dola za Kimarekani bilioni
45. Mfuko huo mpya utaruhusu mataifa matajiri zaidi kuelekeza akiba zao
za dharura ili kusaidia nchi zilizo hatarini kushughulikia changamoto za
muda mrefu. Kwa hivi sasa, IMF inatoa kiwango cha chini cha riba
kusaidia nchi kukabiliana na changamoto za muda mfupi, kama vile mfumuko
wa bei na changamoto za muda za kifedha. Ufadhili huo utayalenga
mataifa yaliyoathiriwa zaidi na janga la corona.
Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii