Mawaziri wakuu wa Finland na Sweden jana walikutana mjini Stockholm kujadili usalama wa kikanda kutokana na vita vinavyoendelea nchini Ukraine. Waziri mkuu wa Finland Sanna Marin na Magdalena Andersson wa Sweden wamesema serikali zao zinaweza kubadili sera za miongo kadhaa juu ya kujiunga na jumuiya ya kujihami ya NATO. Finland inatarajiwa kufanya uamuzi ndani ya wiki hii. Wanachama wote 30 wa NATO watahitaji kuidhinisha uanachama wa kila nchi, uamuzi unaoweza kuchukua hadi mwaka mmoja. Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg amesema mlango wa uanachama bado uko wazi. Wachambuzi wengi wanatarajia kwamba nchi hizo mbili zitawasilisha maombi ya pamoja. Msemaji wa Ikulu ya Urusi Kremlin Dmitry Peskov amesema ikiwa Finland itajiunga na NATO, Urusi itajaribu kusawazisha hali hiyo.