Waziri wa Habari, Mawasiliano na
Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nauye amezikumbusha taasisi za TANROAD
na TARURA kuweka majina ya barabara ili kurahisisha Operesheni ya Anwani
za Makazi
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua mwenendo wa
utekelezaji wa Operesheni hiyo Mkoani Kilimanjaro, Waziri Nape
amesisitiza kuwa iko hatari ya ukiritimba unaoweza kufanywa na baadhi ya
watu kwa kujiita majina ya mitaa yote na barabara kwa kigezo cha
kuchangia fedha za utekelezaji wa zoezi la uwekeji wa Anwani za Makazi.
“Haya
ni maelekezo yaliyotolewa na Waziri Mkuu kwamba TANROAD na TARURA
kwasababu barabara zote ni za kwao wahakikishe wanaweka majina ya hizi
barabara ili isaidie kasi ya kukamilisha zoezi hili na mie naomba
niwakumbushe watekeleze maelekezo kwa kuweka majina ya hizi barabara ili
kuzipunguzia mzigo halmashauri na kuongeza kasi ya utekelezaji wa
operesheni .” Amesema Waziri huyo
Ameongeza kuwa, viongozi na
wananchi wanatakiwa kuwa makini katika kuweka majina ya mitaa kwa kuwa
kuna wadau wanajitolea, wanachangia fedha zao lakini ni vizuri majina
yawe yenye uzalendo na yanayoendana na uhalisia wa nchi yetu yakiwemo
majina ya viongozi pamoja na watu mashuhuri.
Katika hatua
nyingine, Waziri Nape ameonesha kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa
operesheni hiyo katika Mkoa wa Kilimanjaro ambapo utekelezaji wake
umefikia asilimia 99.1.