Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa wiki ijayo limepanga kukutana katika kikao kingine kujadili hali ya kibinadamu nchini Ukraine,ikiwa ni juhudi za kuendelea kuitia mbinyo Urusi licha ya kutumia kura yake ya turufu katika baraza hilo. Kikao hicho kitafanyika baada ya jana Jumatatu baraza hilo kuijadili hali ya wanawake na watoto nchini Ukraine. Mkutano huo wa wiki ijayo kwa mujibu wa mwanadiplomasia ambaye hakutaka kutajwa jina,umependekezwa na Ufaransa pamoja na Mexico na utajikita kwenye kuangalia suala la wakimbizi,raia wa nchi za ulimwengu wa tatu pamoja na biashara ya usafirishaji watu. Katika kikao cha jana Jumatatu kilichopendekezwa na Marekani na Albania,balozi wa Albania katika Umoja wa Mataifa Ferit Hoxha alisema washirika wa Umoja huo wataendelea kulaani uvamizi wa 24 Februari wa Urusi nchini Ukraine hata ikiwa Moscow imeliteka nyara baraza la usalama la nguvu yake ya kura ya turufu,na kulizuia kutowa usalama kwa Ukraine.