Baraza kuu la Umoja wa Mataifa linapiga kura hii leo ya uwezekano wa kuisimamisha Urusi kwenye baraza lake la haki za binaadamu. Hatua hiyo ilianzishwa na Marekani kufuatia kugundulika kwa mamia ya miili baada ya Urusi kuondoa wanajeshi wake kwenye miji iliyo karibu na mji mkuu wa Ukraine, Kiev. Msemaji wa Baraza Kuu la Umoja huo Paulina Kubiak amesema jana kwamba kikao hicho cha dharura cha baraza kuhusu Ukraine kitarejea majira ya saa nne za asubuhi leo wakati azimio la kusimamisha uanachama wa Urusi litakapopigiwa kura. Balozi wa Marekani kwenye Umoja huo Linda Thomas-Greenfield alisema siku ya Jumatatu kwamba wanaamini wanajeshi wa Urusi walifanya uhalifu wa kivita nchini Ukraine na kwamba Urusi inatakiwa kuwajibishwa.