• Jumatatu , Agosti 11 , 2025

Aliyekuwa meneja wa PSSSF na wenzake wasomewa upya mashtaka yao

Aliyekuwa Meneja wa Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) wa mkoa wa Temeke, Rajabu Kinande na wenzake wanne wamesomewa mashtaka upya katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala baada ya mshtakiwa Rose Mabaka kufariki dunia.

Mbali na Kinande washtakiwa wengine ni Dk Ashura Kapera (37), Farida Mbonaheri (34), Mohamed Miraji (48) na Msafiri Raha.

Akisoma hati ya mashtaka Wakili wa Serikali, Michael Ng'hoboko mbele ya Hakimu Mkazi, Fadhil Luvinga ameeleza shauri limekuja kwa ajili ya washtakiwa hao kusomewa upya mashtaka yanayomkabili baada ya mshtakiwa Mabaka kufariki dunia.

Katika kesi ya msingi inadaiwa kati ya Juni 16, 2020 mtaa wa Gerezani Wilaya ya Ilala washtakiwa hao kwa pamoja walivunja na kuingia kwenye duka na kuiba vitu mbalimbali vyenye thamani ya Sh60.8 milioni mali ya Mohamed Soli, Anwar Hemed, Rashidi Hassan na Salehe Seleman

Hata hivyo washtakiwa hao walikana makosa yanayowakabili.

Ng'hoboko alidai upelelezi umekamilika na aliiomba mahakama hiyo ipange tarehe nyingine kwa ajili ya ushahidi.

Baada ya maelezo hayo hakimu Luvinga amesema washtakiwa hao wataendelea na dhamana zao na aliahirisha shauri hilo hadi Aprili 28, 2022 Kwa ajili ya kuanza na ushahidi.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii