Marekani kupendekeza azimio jipya la kuilaani Korea Kaskazini

Marekani inao mpango wa kuwasilisha muswada wa azimio jipya katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, la kuiwajibisha Korea Kaskazini baada ya nchi hiyo kufanya jaribio jingine la makombora yenye uwezo wa kusafiri kutoka bara moja hadi jingine. Sung Kim, mjumbe maalumu wa Marekani kuhusu Korea Kaskazini amesema jaribio hilo ni ukiukaji wa wazi wa maazimio mengine kadhaa ya Umoja wa Mataifa. Hayo Kim ameyasema mjini Washington katika mkutano na mjumbe wa Korea Kusini kuhusu masuala ya rasi ya Korea, Noh Kyu-duk. Tarehe 24 Machi, Korea Kaskazini ililifanyia majaribio kombola lake lenye uwezo mkubwa zaidi, ambalo linaweza kupiga shabaha mashariki mwa Marekani likibeba bomu la nyuklia. Korea Kaskazini hapo jana iliionya Korea Kusini, ikisema ikiwa inataka vita, jeshi la Korea Kaskazini liko tayari.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii