Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky ameonya kuwa hali mbaya zaidi inaweza kutokea wakati Urusi ikielekeza tena nadharia yake kusini na mashariki mwa nchi hiyo, katika juhudi za kuiunganisha Rasi ya Crimea inayoikalia kimabavu na majimbo yanayotaka kujitenga ya Donetsk na Lugansk. Mkuu wa majeshi ya Ukraine amesema Urusi ilitarajiwa kuwakusanya takribani askari wa akiba 60,000. Miripuko ya mabomu imesikika mapema leo kwenye miji ya Kherson na Odesa eneo la kusini, huku ving'ora vya mashambulizi ya anga vikisikika eneo la mashariki. Duru za kijasusi za jeshi la Uingereza zimeeleza kuwa mapigano makali yameendelea kwenye mji wa Mariupol wakati ambapo vikosi vya Urusi vinajaribu kuuteka mji huo wa bandari. Shughuli za kusafirisha misaada kati ya mji wa Chernihiv na Kiev zilitarajiwa kuanza tena leo asubuhi. Gavana wa Chernihiv, Viacheslav Chaus amesema barabara za pande zote mbili zitafunguliwa na kutakuwa na kikomo cha uzito wa tani tano na foleni za magari zinatarajiwa kuwepo kwenye baadhi ya maeneo.