Mamlaka ya Palestina imesema Wapalestina wawili wameuwawa leo wakati majeshi ya Israel yalipofanya uvamizi katika Ukingo wa Magharibi. Hii ni baada ya msururu wa mashambulizi yaliyofanyika nchini Israel, wizara ya afya ya Palestina imesema vijana wawili mmoja akiwa na umri wa miaka 17 na mwengine miaka 23 wameuwawa na majeshi ya Israel yalipovamia Jenin na watu wengine 15 wamejeruhiwa. Jeshi la Israel kwa upande wake linasema wanajeshi wake walishambuliwa walipojaribu "kuwakamata washukiwa wa ugaidi" huko Jenin na kudai kwamba mmoja wa wanajeshi wake amejeruhiwa. Machafuko hayo yamefanyika huku kukiwa na mivutano kuelekea mwezi wa mfungo wa Waislamu wa Ramadhan kufuatia mashambulizi nchini Israel ambapo Waisraeli 11 wameuwawa katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.