Ndege mbili za Korea Kusini zimegongana angani wakati wa mazoezi na kuanguka karibu na kambi yake, na kuua watu wote wanne waliokuwemo ndani yake. Kulingana na mamlaka ya kijeshi, ndege hizo za mafunzo chapa KT-1 zilianguka karibu na mji wa Sacheon, takriban kilomita 300 kusini mwa mji mkuu Seoul. Ajali ya leo ndiyo tukio la karibuni zaidi linalohusisha ndege za jeshi la anga la Korea Kusini kwa mwaka huu. Mnamo mwezi Januari, rubani wa jeshi la anga alikufa katika ajali ya ndege ya kivita ya F-5. Tukio hilo lilitokea muda mfupi baada ya taifa hilo kusimamisha matumizi ya ndege zake zote za kisasa za F-35, baada ya mojawapo kutua kwa dharura kutokana na kasoro za kimfumo.