Urusi imesema imetangaza kusitisha kwa muda mapigano kwenye mji wa Mariupol ili kuruhusu raia kuondoka kwenye eneo hilo. Kamanda wa Urusi, Meja Jenerali Mikhail Mizintsev amesema mapigano yatasitishwa kuanzia leo saa nne asubuhi kwa saa za Ukraine. Mpango huo utawaruhusu raia kuondoka kutoka Mariupol kwenda Berdyansk na kisha kuelekea kwenye mji wa Zaporizhzhia. Hata hivyo, Umoja wa Mataifa na Shirika la Msalaba Mwekundi yamesema Ukraine ilipewa hadi muda wa leo saa 12 asubuhi kuthibitisha kuhusu mpango wa kusitisha mapigano. Nchi hizo mbili mara kwa mara zimekuwa zikitupiana lawama kwa kukiuka juhudi za kuwaondoa raia kutoka kwenye mji huo wa bandari katika Bahari ya Azov. Majaribio mengi yaliyowekwa awali ya kuanzisha njia za kiutu Mariupol yameshindwa. Mariupol ni moja ya malengo makuu ya operesheni za Urusi wakati ikijaribu kuiteka pwani ya Azov.