Zelensky ana mashaka na ahadi ya Urusi kupunguza mashambulizi

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky amesema mazungumzo ya amani kati ya wapatanishi wa nchi yake na Urusi yameonesha mwelekeo mzuri, ingawa ameonya kuwa Urusi haiwezi kuaminiwa. Baada ya mazungumzo ya jana yaliyofanyika Istanbul, Uturuki, Urusi ilitangaza kuwa itapunguza kwa kiasi kikubwa operesheni za kijeshi karibu na mji mkuu wa Ukraine, Kiev na mji wa kaskazini wa Chernihiv. Akizungumza jana usiku kwa njia ya video, Zelensky amesema vitendo vya ujasiri na madhubuti vya wanajeshi wa Ukraine viliilazimisha Urusi kupunguza operesheni zake karibu na miji hiyo. Amesisitiza kuhusu Ukraine kutoamini matamshi ya wawakilishi wa nchi ambayo bado inaendelea kufanya mashambulizi na kuwaangamiza. Aidha, Zelensky amesema hapawezi kuwepo na mazungumzo ya kuiondolea Urusi vikwazo, hadi hapo vita vitakapomalizika. Wizara ya Ulinzi ya Marekani imesema inaamini kuwa baadhi ya wanajeshi wa Urusi tayari wameanza kuondoka Ukraine. Marekani na nchi nyingine zimeelezea mashaka yao kutokana na tangazo la Urusi na wanasubiri kuona kitakachotokea.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii