Mrembo Mkenya Hataki kuwa Mama Akidai Watoto ni Mzigo.

Mwanamke mmoja Mkenya amejitokeza na kusema kwamba hataki kupata mtoto wakati wowote maishani mwake.
Ebbie Weyime, 34, alisema yeye ni mwanamke wa Kiafrika anayefurahia maisha yake bila kuwa na mtoto na hatakii kuzaa katika siku za usoni.
Kulingana na mwanamke huyo, watoto ni mzigo akisema afadhali kuwa mwanamke asiye na mtoto badala ya kuzaa mtoto ambaye hataweza kumtunza.
"Sina mtoto na sitaki kuwa nao wakati wowote katika maisha yangu. Mimi ni mwanamke wa Kiafrika mwenye furaha sana bila mtoto," alisema.
Mwanablogu huyo wa YouTube anayetumia akaunti ya The ChildFree Kenyan, alifichua kwamba alifanyiwa upasuaji wa kukata vibomba vya uzazi mnamo Oktoba 2020, kwa vile alijua kwamba hataki watoto maishani mwake.
"Ilikuwa hadi Julai 2020, nilipogundua kuwa nina mimba! Kwa hiyo nilitoa mimba na miezi mitatu kamili baadaye, nilifanyiwa upasuaji wa kukata vibomba vya uzazi (BTL). Sikutaka kuwa kwenye hatari ya kupata ujauzito mwingine. Nilijua tayari sitaki mtoto, kwa hivyo mbona ujihatarishe?" alisema kwa kujiamini
Alidai kuwa watu wamekuwa wakikosoa uamuzi wake kuwa wa mtu mbinafsi na asiyependa watoto.
"Watu wengi hukosea kutokuwa na watoto kumaanisha kuwachukia watoto wa watu na kuwasukuma mbali nao. Kwa kweli, ninawapenda watoto sana. Lakini kwa sababu tu unapenda aiskrimu haimaanishi kwamba lazima ununue mashine ya aiskrimu," alidai.
Weyime ambaye ni mwanzilishi wa Grace Cup, alisema kuwa wazazi wake walikuwa kinyume na uamuzi wake, lakini alilazimika kufanya hivyo kwa faragha kwani alijifanyia mwenyewe wala si wazazi wake.
"Yalikuwa mazungumzo magumu kuwa nayo, haswa wazazi wangu wakiwa Waafrika, siku zote walitarajia watoto wao wawape wajukuu. Kwa hiyo nilitoka kwa faragha bila kuwaambia wazazi wangu kwa sababu tayari walikuwa wamekataa," alisema.
Mfanyabiashara huyo ambaye pia ni mwanamitindo, alisema kwa sasa yuko katika uhusiano wa kimapenzi na wanaume wawili ambao wote wanaheshumu uamuzi wake wa kutokuwa na watoto.
“Niko katika mahusiano na wanaume wawili, mimi si mwanamke wa mwanamume mmoja, maana yake siamini katika ndoa ya mke mmoja, mimi siamini katika mwanaume mmoja mwanamke mmoja hivyo ndio sababu nadeti wanaume wawili na wote wawili wanafahamu na wako sawa nalo."
"Wanaume wote wawili wana watoto, lakini hawataki kuwa na zaidi. Mtu ameshafanyiwa vasektomi tayari, kwa hiyo ana uhakika wa chaguo lake. Huyo mwingine kwa hakika hataki watoto pia, kwa hivyo ndio, nina uhusiano wa furaha," alisema.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii