Kenya na Jersey zimetia saini mkataba utakaowezesha zaidi ya KSh 450 milioni zilizoibwa na kufichwa kwenye akaunti za nje ya nchi kurejeshwa.
Pesa hizo zilifichwa kwenye akaunti za nje ya nchi na maafisa wa zamani wa serikali Chris Okemwa (waziri wa kawi) na Samuel Gichiru (bosi wa zamani, wa Kenya Power).
Hii ni mara ya kwanza pesa zilizofichwa nje ya nchi kurejeshwa kupitia Mfumo wa Kurudisha Mali zilizotokana na Ufisadi na Uhalifu hadi Kenya(FRACCK).
“Kurejeshwa kwa Sh450 milioni kunaashiria kwamba hakuna mahali popote duniani ambapo wafisadi wanaweza kuficha nyara zao. Kenya imejitolea kufanya kazi na washirika kama vile Uingereza, Uswizi, na Jersey, ili kutimiza azma ya FRACCK,” alisema Balozi ya wa Kenya nchini Uingereza, Manoa Esipisu wakati wa kutia saini mkataba huo.
Balozi Esipisu alisema fedha hizo zilizonyakuliwa zitaelekezwa katika sekta ya afya nchini.
"Matumizi ya fedha zilizorejeshwa yatasaidia sana katika kuharakisha utekelezaji wa mpango wa Huduma ya Afya kwa Wote (UHC) ambayo ni moja ya maeneo muhimu chini ya Ajenda Nne Kuu," alisema.
Kulingana na Mkuu wa Utumishi wa Umma, Joseph Kinyua, kuibuka kwa janga la COVID-19 kulihitaji kuwekeza zaidi katika sekta ya afya.
Ripoti iliyotolewa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) ilionyesha kuwa zaidi ya Wakenya 400 wakiwemo maafisa wa serikali wana akaunti za benki nje ya nchi.