Umoja wa Mataifa wachunguza ripoti za makaburi ya watu wengi Libya

Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa wamesema wanajaribu kuthibitisha taarifa za kuwepo makaburi ya watu wengi katika vituo vya kuwasafirisha wahamiaji nchini Libya. Umoja huo pia umesema umepokea taarifa za kuwepo ubakaji, utesaji na mauaji. Wahamiaji wamewaambia wachunguzi wa Umoja wa Mataifa kwamba makaburi ya watu wengi yako kwenye mji wa Bani Walid. Hakuna maelezo maalum yaliyotolewa kuhusu idadi ya watu waliozikwa katika makaburi hayo. Umoja wa Mataifa umesema umeteua timu ya wataalamu kuchunguza uhalifu huo. Ripoti ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa imeonyesha vitendo vya kinyama vinavyofanywa dhidi ya wahamiaji walioko mikononi mwa watu wanaofanya biashara haramu ya kuuza binaadamu, ikiwemo kuunguzwa sehemu zao za siri. Libya ambayo imekuwa kwenye machafuko tangu mwaka 2011, ni kituo kikuu cha usafiri chenye shughuli nyingi za Waafrika wanaojaribu kuvuka Bahari ya Mediterrania kuelekea barani Ulaya.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii