Kiongozi wa kilichokuwa chama tawala Burkina Faso akamatwa

Kiongozi wa kilichokuwa chama tawala nchini Burkina Faso, Alassane Bala Sakande amekamatwa baada ya kukosoa mazingira ya kushikiliwa rais wa zamani wa nchi hiyo, Roch Marc Christian Kabore. Mawakili wa Sakande wamesema mteja wao alikamatwa jana na polisi akiwa nyumbani kwake na kupelekwa kwenye kambi ya polisi ya Paspanga. Kwa mujibu wa mawakili hao, Sakande amekamatwa baada ya kuutaka utawala wa kijeshi wa Burkina Faso ulio chini ya Luteni Kanali Paul-Henri Sandaogo Damiba kumuachilia huru mara moja Kabore ambaye aliondolewa madarakani katika mapinduzi ya kijeshi mwezi Januari na anaendelea kuwekwa katika kizuizi cha nyumbani. Sakande aliyatoa matamshi hayo Machi 24 mbele ya waandishi habari wakati wa mkutano wa chama chake cha MPP. Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Uchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS zote timetaka Kabore aachiliwe huru.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii