Kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS limekiri kuhusika na shambulizi nchini Israel ambalo limewaua wanajeshi wawili na kuwajeruhi wengine 10. Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na IS kupitia mtandao wa Telegram. Awali maafisa wa usalama wa Israel walisema kuwa Waarabu wawili waliokuwa na silaha jana waliwaua watu wawili kwenye mji wa Hadera, ulioko umbali wa kilomita 50 kaskazini mwa Tel Aviv, kabla na wao kuuawa kwa kupigwa risasi. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken aliyeko ziarani nchini Israel amelaani vikali shambulizi hilo. Blinken ameandika katika ukurasa wake wa Twitter akisema wanasimama na washirika wao wa Israel na kwamba Marekani inatuma salamu za rambirambi kwa wahanga. Amesema vitendo hivyo vya ukatili na mauaji havina nafasi katika jamii.