Abiria wote 132 waliokuwa wamepanda ndege chapa MU5735 mashariki mwa China wamethibitishwa kufa baada ya ndege hiyo kuanguka.
Mamlaka ya anga ya China CAAC imethibitisha taarifa hizo. Naibu mkurugenzi wa CAAC Hu Zhenjiang amewaambia waandishi wa habari kwamba hakuna dalili yoyote ya manusura kwenye eneo la ajali lililoko katikati ya msitu mkubwa katika eneo la Guangxi karibu na jiji la Wuzhou.
Abiria 120 walitambuliwa kupitia vipimo vya vinasaba wakati familia za wahanga zikiwa zinasubiri kwa siku kadhaa kusikia taarifa za ndugu zao kuokoloewa na vikosi vya uokozi.
Mamlaka bado ziko njia panda katika kung’amua chanzo cha ajali hiyo ambayo ni mbaya zaidi kutokea nchini China katika kipindi cha karibu miaka 30.