Kifaa cha kunasa sauti kwenye ndege ya abiria ya China kimepatikana

Wuzhou,Afisa wa mamlaka ya usafiri wa anga ya China amesema wachunguzi wamepata kile wanachoamini ni kijisanduku cheusi, kifaa cha kunasa sauti kwenye chumba cha marubani kwenye ndege ya abiria ya China iliyoanguka kusini mwa nchi hiyo. Mkurugenzi wa mamlaka ya usafiri wa anga ya China Zhu Tao, amesema kifaa hicho kitatumwa mjini Beijing kwa ajili ya kuchunguzwa. Akizungumza na waandishi wa habari, Tao amesema kuwa kijisanduku hicho kimeharibika sana lakini wachunguzi wanaangalia iwapo kitasaidia katika kubaini kilichosababisha ajali hiyo. Kifaa hicho ni muhimu katika uchunguzi wa kubaini chanzo cha ajali hiyo. Picha zilizotolewa na shirika la habari linalomilikiwa na serikali CCTV zilionyesha wafanyikazi wakikiweka kifaa cha rangi ya chungwa kwenye mfuko wa plastiki. Ndege ya shirika la China Eastern 5735, iliyokuwa imebeba abiria 123 na wafanyikazi wake 9 ilianguka mnamo siku ya Jumatatu katika jimbo la Guangxi.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii