Ketanji Brown Jackson, aliyeteuliwa na Rais wa Marekani Joe Biden kuhudumu katika mahakama ya juu zaidi nchini Marekani, amejitetea juu ya kuwawakilisha wafungwa wa gereza la Guantamano Bay. Ketanji pia amekanusha madai yaliotolewa na wabunge wa Republican kwamba alionyesha huruma katika kesi za ponografia za watoto. Mbele ya kikao cha kamati ya sheria katika bunge la seneti, Ketanji ameahidi kuwa mwanasheria wa kujitegemea na ambaye hatatia maoni yake binafsi katika maamuzi ya kisheria. Mwanasheria huyo aliteuliwa na Rais Biden mnamo mwezi Februari kuhudumu katika mahakama ya juu zaidi nchini Marekani, ambapo iwapo ataidhinishwa na bunge la seneti, atakuwa mwanamke wa kwanza mweusi kujiunga na mahakama hiyo ya juu zaidi nchini Marekani. Amehudumu kuanzia mwaka jana kama jaji wa mahakama ya rufaa, na kabla ya hapo alihudumu kama jaji wa mahakama ya wilaya kwa muda wa miaka minane.